Jumatatu 26 Januari 2026 - 07:00
Kuitambua dunia mpya na mikondo mipya inayoibuka ni jukumu letu kuu / Hawza ni kiongozi wa fikra na mawazo ya Uislamu katika zama za sasa

Hawza/ Ayatollah A’raafi, akibainisha kuwa taasisi ya dini ina majukumu mazito sana juu yake, alisisitiza akisema: jukumu letu la kwanza na la msingi kabisa ni kuitambua dunia mpya na mikondo mipya inayoibuka, kwa sababu bila utambuzi huo, haitawezekana kuchukua hatua yoyote yenye athari.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Alireza A’raafi katika mkutano na mkurugenzi pamoja na wajumbe wa Taasisi ya Fikra ya Kituo cha Usimamizi wa Hawza, akirejelea fadhila na hazina za kiroho zilizo mahsusi kwa mwezi mtukufu wa Shaaban, alisema: Mwenyezi Mungu Mtukufu awajalie Waumini wote tawfiki ya kunufaika na baraka za mwezi huu kwa ajili ya kujikurubisha Kwake, na kuchukua hatua kubwa zaidi katika kusambaza maarifa ya dini nchini Iran na duniani kote.

Munajati  Shaabania na Swala za Shaabania; mabawa mawili ya kupaa kuelekea kwa Mwenyezi Mungu

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini, akiendelea kusisitiza umuhimu wa misingi miwili ya msingi ya “Tawhidi” na “Wilaya” kama mabawa mawili ya kupaa katika mwezi huu, alisema: Munajati Shaabania na Swala za Shaabania, kwa pamoja, zinaandaa njia iliyo laini na wazi kwa ajili ya safari ya kiroho na kumkaribia Mola.

Ayatollah A’raafi aliitaja Munajati ya Shaabania kuwa ni kielelezo cha fikra ya juu kabisa ya Tawhidi safi na mfumo wa safari ya kiroho kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Akirejelea ukubwa na kina cha maana za munajati hii, alisema: Ndani ya munajati hii kuna ulimwengu ulio changamano sana na wa kuvutia mno.
Akiashiria kurudiwa kwa neno “Ewe Mola wangu (Ilahi)” zaidi ya mara arobaini katika munajati hii, alibainisha kuwa jambo hili ni kufunguliwa kwa mlango kuelekea safari ya kiroho. Munajati ya Shaabania inaonyesha mfumo kamili wa suluki (tabia ya kiroho), inaonesha mwanzo wa safari, hatua zilizopigwa, maeneo yaliyovukwa na vilele vinavyomwongoza mwanadamu kuelekea uongofu. Kila mara neno “Ilahi” linapotamkwa kwa umakini, ni hatua kubwa inayochukuliwa katika kujitambua, kumkaribia Mwenyezi Mungu na kuimarisha Tawhidi.

Swala za Shaabania; mfumo unaokamilisha Munajati ya Shaabania

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini aliielezea Swala ya Shaabania kuwa ni mfumo unaokamilisha Munajati ya Shaabania, akisema: Katika Swala ya Shaabania, kunajadiliwa kipindi cha “utambuzi wa Utume” na “utambuzi wa Wilaya”, ambacho kinakamilisha mtazamo safi wa Tawhidi uliopo katika munajati.

Ayatollah A’raafi, akiendelea, alisema kuwa si tu kwamba sisi wenyewe tunapaswa kuzingatia maana hizi za kina, bali lililo gumu zaidi na muhimu zaidi ni kuzihamisha kwa wengine. Alisisitiza: Falsafa nzima ya uwepo wa Hawza ya Elimu ya Dini ni kuwasilisha maarifa haya safi na matakatifu kwa jamii, na wanachama wa taasisi ya fikra ni miongoni mwa nguzo muhimu katika kutekeleza harakati hii yenye thamani.

Umuhimu wa kuitambua dunia mpya kwa usahihi

Ayatollah A’raafi, akirejelea mabadiliko makubwa na ya kushangaza katika uwanja wa kimataifa, alisema: Dunia mpya na mazingira yanayotuzunguka katika kipindi cha miaka miwili iliyopita yana tofauti za kimsingi ikilinganishwa na zamani. Ndani ya mabadiliko haya kuna fursa kubwa pamoja na vitisho vikubwa na vya hatari sana vinavyohitaji uchambuzi wa kina kutoka Hawza ya Elimu ya Dini na maeneo yote yenye wajibu.

Kubaini fursa, changamoto, vitisho na majukumu katika hali ya sasa

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza za Elimu ya Dini alisema kuwa kubaini fursa, changamoto, vitisho na majukumu katika hali ya sasa ni jambo la lazima. Akichambua matukio ya hivi karibuni, alisema: Tangu mwanzoni mwa matukio yaliyotokea miaka miwili iliyopita, katika uchambuzi nilioutoa katika mikutano mbalimbali, nilisisitiza kwamba wimbi jipya limeibuka, ambalo ni tofauti kabisa na mawimbi yote yaliyotangulia na ni zito sana.

Ni mwelekeo ambao utaendelea, na mkondo wa Mapinduzi, Hawza na taasisi ya dini lazima viwe na maandalizi kamili kwa ajili yake.

Ayatollah A’raafi alisisitiza kuwa, matukio na masuala ya sasa, ikiwemo vita, machafuko na masuala ya msingi zaidi, hayawezi kulinganishwa na vipindi vya zamani. Alisema: Hali hii ni tofauti kabisa na nyakati zote zilizopita na ni nzito sana. Mimi ni mtu ambaye tangu ujana wangu nilishiriki katika masuala ya Mapinduzi, na nashuhudia kwamba hali ya sasa ni tofauti na vipindi vyote vilivyopita. Pamoja na vitisho hivi, bado nina matumaini makubwa juu ya uwepo wa fursa kubwa, lakini sipuuzi ukubwa wa vitisho na changamoto zilizopo.

Hawza ya Elimu ya Dini ni kiongozi wa fikra na mawazo ya Uislamu katika zama za sasa

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini alisema kuwa taasisi ya dini ina majukumu mazito sana, akibainisha: Tuna wajibu wa kuitumikia dini, na Hawza ya Elimu ya Dini lazima icheze nafasi yake kama kiongozi wa fikra na mawazo ya Uislamu na Mapinduzi katika dunia ya leo.

Ayatullah A'rafi alisema: Jukumu letu la kwanza na muhimu zaidi ni kuitambua dunia hii mpya na mikondo mipya inayoibuka, kwa sababu bila utambuzi huu, haitawezekana kufanya hatua yoyote yenye athari.

Umuhimu wa mawasiliano endelevu kati ya taasisi ya dini, wanazuoni wa dini na jamii

Ayatollah A’raafi alisisitiza umuhimu wa mawasiliano endelevu kati ya taasisi ya dini, wanazuoni wa dini na jamii, akisema: Hawza ya Elimu ya Dini na taasisi ya wanazuoni wa dini katika hali ya sasa, kwa baraka ya Mapinduzi ya Kiislamu, zinakabiliwa na fursa za kihistoria zisizo na mfano, na wakati huo huo zinakabiliwa na changamoto kubwa sana na madhara yanayoitishia taasisi hii.

Aliongeza kuwa: Uchambuzi wa kina wa suala hili na kutoa suluhisho kwake ni jambo muhimu sana na la msingi, ambalo taasisi za utafiti zinapaswa kulishughulikia kwa umakini zaidi. Ingawa hatua zilizochukuliwa hadi sasa hazitoshi, na kuna haja ya kazi sahihi zaidi na ya kina. Hili linahitajika katika ngazi ya jamii kwa ujumla, hasa kwa vijana, na pia katika ngazi ya wasomi na vyuo vikuu. Aidha, ni lazima kuangalia mtazamo wa Waumini walioko nje ya nchi kuhusu sisi na ni masuala gani yanayozunguka katika fikra zao.

Hawza iitambue nafasi yake katika mfumo wa fikra za kimataifa

Ayatollah A’raafi, akiendelea, alisisitiza umuhimu wa kuitambua nafasi ya kimataifa ya Hawza, akisema: Ni lazima tuone dunia inatuonaje, na sisi tuko katika nafasi ipi hasa ndani ya mfumo wa fikra za kimataifa. Utambuzi sahihi wa nafasi hii ni muhimu kwa ajili ya mipango ya baadaye na harakati zenye ufanisi za Hawza ya Elimu ya Dini.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini, akirejelea hali ya sasa ya mfumo wa elimu na fikra duniani, alisema: Kuzingatia nafasi yetu katika mfumo wa elimu na mawazo ya dunia, na kufanya jitihada za kuiboresha, ni mhimili muhimu sana unaopaswa kuzingatiwa kwa uzito na taasisi za utafiti na idara mbalimbali ili ziweze kuwa hai na tendaji zaidi katika nyanja hizi.

Kuimarishwa kwa kiungo cha mawasiliano na wataalamu wa fikra

Alisisitiza umuhimu wa kuunda kiungo cha mawasiliano na kundi la wataalamu wa fikra, kwakusema: Kusikiliza sauti ya wataalamu ni jambo la msingi sana. Kwa bahati nzuri, kazi hii imeanza katika taasisi ya fikra na hatua nzuri zimechukuliwa. Uchambuzi, ukusanyaji na uundaji wa benki ya mawazo pia ni miongoni mwa majukumu ya taasisi ya fikra, na kadiri benki hii ya mawazo inavyoimarishwa, ndivyo kazi zitakavyokomaa zaidi, taarifa zitakavyokuwa sahihi, na matumaini ya maendeleo yataongezeka miongoni mwa wadau.

Umuhimu wa kutumia uwezo wote uliopo

Ayatollah A’raafi alisisitiza umuhimu wa kutumia uwezo wote uliopo, akisema: Kwa kawaida, taasisi za fikra na utafiti zina mamia ya masuala, na kwa uwezo wao mdogo haziwezi kuyachambua yote na kuyafikisha kwenye matokeo. Hivyo, ni lazima mipango ifanywe ili meza ya utafiti ipanuliwe na mitandao zaidi iundwe; mitandao yenye uwezo wa kukusanya na kusimamia masuala mbalimbali.

Mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza aliongeza: “Uundaji wa mitandao na minyororo ya uwezo” kwa ajili ya kutatua matatizo ni jambo muhimu sana linalopaswa kutekelezwa katika mfumo wa taasisi za fikra na tafiti.

Umuhimu wa “usimulizi wa hoja” na “ujenzi wa mijadala”

Mjumbe wa wanazuoni wa Baraza la wasimamizi, huku akisisitiza umuhimu wa “usimulizi wa hoja” na “ujenzi wa mijadala” kuhusu hatua zilizotekelezwa au zinazoendelea, alisema: Ujenzi wa mijadala ni jambo la msingi sana.

Mkurugenzi wa Hawza za Elimu ya Dini, akiendelea, alirejelea moja ya masuala muhimu na ya kimkakati, akasema: Mada ya “akili bandia” na “sayansi za utambuzi” ni miongoni mwa masuala yanayobadilisha mifumo yetu yote na kuunda dunia tofauti kabisa. Teknolojia kama akili bandia si tena suala la zana rahisi; teknolojia hizi sasa zimekuwa washirika wa binadamu na kwa kasi kubwa, katika nyanja nyingi, zimeanza hata kumpiku binadamu mwenyewe.

Ayatollah A’raafi alisema kuwa, mabadiliko haya yanayumbisha na kubadilisha dhana zetu nyingi, akasisitiza: Kujiandaa kukabiliana na matukio haya ni jambo la uhai na kifo. Kwa mtazamo wangu, ni lazima tufanye kazi nzito zaidi na za kina zaidi katika uwanja huu ili tuweze kusimamia changamoto na fursa zinazotokana na mabadiliko haya makubwa.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha